Kutoa Mafunzo Kwa Wafungwa
Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), inaadhimisha miaka 30 tokea ilipoanzishwa mwaka 1994.
Maadhimisho hayo yanakwenda sambaba na miaka 50 ya utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi kupitia taasisi mbalimbali za Serikali nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore anasema kwamba, maadhimisho hayo yana malengo makuu matatu, ikiwemo kutambua na kusherehekea mchango wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi katika maendeleo ya Taifa.
Pia anasema wanapitia safari hiyo ya miaka 30 kwa ajili ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza na fursa zilizopo kwa maendeleo zaidi ya sekta hiyo.
Vile vile kujadili mwelekeo wa sekta ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kipindi kijacho kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mafunzo yamwaka 2014, toleo la 2023.
Kasore anasema, maadhimisho hayo yatawezesha kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine muhimu wa maendeleo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, maadhimisho hayo yatafanyika katika ngazi ya vyuo na kanda mbalimbali kote nchini.
“Hata hivyo, kilele cha maadhimisho haya kitaadhimishwa kwa siku nne, kuanzia Machi 18 hadi 21, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam,” anasema.
Katika kipindi cha maadhimisho hayo, anaeleza kuwa kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho ya kazi, ubunifu wa teknolojia kutoka kwenye vyuo vya ufundi stadi na wadau wake,
Programu za mafunzo na huduma mbalimbali zitolewazo na VETA na wadau wake.
“Wengi wanatambua kuwa VETA ni familia ya wabunifu. Tuna ubunifu mwingi wa walimu, wanafunzi na wahitimu wetu. Kwa hiyo itakuwa fursa kubwa kwa watu kujionea ubunifu kutoka kwenye vyuo vyetu,” anasema.
Pia anasema kutakuwa na mashindano ya Ujuzi yatakayowashirikisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kuonesha umahiri katika stadi mbalimbali, kwamba wanafunzi wa VETA wataonesha umahiri wao kupitia mashindano hayo.
Mengine yatakayokuwepo ni kongamano la wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali kuhusiana na elimu na Mafunzo ya ufundi stadi.
Anasema vilevile kutakuwepo na utoaji wa tuzo kwa taasisi, wadau, na wahitimu waliochangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Katika ngazi ya Kanda, anasema kwamba vyuo vyao vilivyopo Katika mikoa mbalimbali nchini kote vitatoa huduma za ufundi zikihusisha matengenezo na ukarabati wa miundombinu katika majengo ya umma au nyumba za familia maskini.
“Tutatumia wanafunzi na walimu wetu kutoa huduma kama vile upakaji rangi kwenye majengo, utandazaji waya za umeme, ukarabati wa miundombinu ya maji na hata uezekaji au ujenzi wa majengo yaliyobomoka,” anasema.
Akizungumzia mafanikio ya mamlaka hiyo anasema, wanapoadhimisha miaka 30 ya VETA, Wanayo mengi ya kujivunia kwani mamlaka hiyo, imepiga hatua kubwa katika kutoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini Tanzania.
Kwa utuaji wa mafunzo hayo, anasema imegusa makundi mbalimbali katika jamii, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Anasema mafanikio hayo wanayojivunia ni pamoja na Ongezeko la Vyuo vya VETA, kwani wakati mamlaka hiyo inaanzishwa, kulikuwa na vyuo 14 vikiwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 1940 tu.
“Sasa tunavyo vyuo 80 vikiwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 83,974 kwa mwaka. Vyuo 65 vinaendelea kujengwa kwenye wilaya mbalimbali nchini ambavyo vinatarajia kuongeza udahili kwa zaidi ya 80,000 kwa mwaka,” anasema.
Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa idadi ya fani za mafunzo. Katika eneo hili, Sekta za mafunzo zimeongezeka kutoka 10 mwaka 1995 hadi 13 mwaka 2025, ikihusisha fani 89 zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Anasema Rasimishaji Ujuzi pia ni miongoni mwa mafanikio Katika mamlaka hiyo, kwani kwa kutambua mchango mchango mkubwa wa mafundi wengi ambao walipata ujuzi pasipo kupitia Mafunzo rasmi,mamlaka hiyo ilianzisha mpango wa kurasimisha ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo.
Kupitia mpango huo zaidi ya mafundi 23,460 wameshafanyiwa tathmini na kutunukiwa vyeti, hivyo ujuzi wao kurasimishwa, kati yao ni wafungwa waliopo magerezani.
“Baada ya kurasimishwa wamenufaika na mambo mengi ikiwemo kupata ajira rasmi badala ya kubaki kama vibarua, kupata zabuni kwenye taasisi binafsi na za umma, kujiendeleza kimafunzo na kupata leseni au vibali maalum vya kuendesha shughuli zao,” anasema.
Mafanikio mengine ni kutoa mafunzo kwa wajasiriamali ili kukuza shughuli zao kwa wale waliopo Katika sekta isiyo rasmi, hivo kupitia mpango huo wajasiriamali 17,811 wamepatiwa mafunzo.
Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa programu za mafunzo ya sehemu ya kazi ambazo ni programu ya uanagenzi pacha na yale jumuishi ya ufund i kwa sekta ya madini.
Anasema kutokana na ubora na umuhimu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi, tafiti zinaonesha kuwa asilimia 67.7 ya wahitimu wa ufundi stadi hupata ajira au kujiajiri baada ya mafunzo yao.
Kwenye mafanikio hakukosi changamoto hivyo mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto ya mahitaji makubwa ya elimu hiyo ikilinganishwa na uwezo wa VETA kutoa mafunzo.
Pia uwepo wa kasi Katika maendeleo ya teknolojia ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa.
Pamoja na changamoto hizo anasema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana nazo, ikiwemo kuongeza bajeti, kushirikiana na sekta binafsi, na kuhakikisha kuwa mtaala wa mafunzo ya ufundi stadi unaenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira.