Na Waandishi Wetu
KITABU cha Utamaduni na Maendeleo Nchini Tanzania, kilichotafsiriwa na walimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU), kimetolewa nchini China.
Walimu waliotafsiri kitabu hicho wa nchini China ni Ma Jun na Ning Yi.
Kutokana na umahiri wake katika kutafsiri, kimewavutia wasomi wengi nchini China.
Hivyo kuwa kivutio katika nchi hiyo, kitabu hicho kimechaguliwa kuwa kimojawapo kati ya vitabu vinavyopendekezwa kwenye Orodha ya Kujumuisha Vitabu vya Kutafsiriwa Mwaka 2024, nchini China.
Tangu ianzishwe orodha ya kuwa na vitabu vilivyotafsiriwa mwaka 2018, kumekuwa na utaratibu wa kupendekeza vitabu vizuri kutafsiriwa kutoka lugha za kigeni kwenda lugha ya Kichina.
Orodha hiyo ya vitabu huchapishwa na Shirika la Uchapishaji wa Sayansi ya Kijamii, hutungwa na kutolewa mara kwa mara, ili kupendekeza kazi za kina na za kuvutia zilizotafsiriwa kwa wasomaji.
Mwaka 2024 ni maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Tanzania.
Urafiki kati ya nchi hizi mbili una historia ndefu. Kitabu cha Utamaduni na Maendeleo Nchini Tanzania kiliandikwa na mwandishi Dkt. Daniel K. Ndagala, kamishna mstaafu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ya Tanzania.
Katika kitabu hicho Dkt. Ndagala amechambua kwa kina kuhusu uhusiano wa kitamaduni na mawasiliano ya kijamii kwa kuzingatia hali halisi ya Tanzania.
Kitabu hicho kinafafanua jukumu muhimu la utamaduni katika ujenzi wa taifa la Tanzania na maendeleo ya jamii, pia kinatoa mapendekezo ya ujumla kuhusu kutekelezwa kwa sera ya utamaduni.
Hivyo kinatoa suluhu kwa ajili ya ustawi wa utamaduni wa Tanzania na kuonyesha mfano bora kwa nchi nyingine zinazoendelea.
Kwa kulinganisha nadharia na uchanganuzi wa kesi halisi, kitabu hicho kinaeleza kwa kina historia na mabadiliko ya sera za utamaduni na miongozo ya maendeleo nchini Tanzania,
Pia kinatoa fursa kwa ulimwengu ili kuelewa sera za utamaduni na maendeleo ya kitamaduni ya serikali nchini Tanzania.
Dkt. Ndagala ni mtafiti, mwandishi na mshauri wa serikali ambaye anazingatia masuala ya utamaduni na maendeleo nchini Tanzania.
Amechapisha vitabu vitatu na tasnifu kadhaa kuhusu utamaduni na sera za utamaduni za Afrika. Anazingatia muingiliano kati ya sera za serikali na jamii za vijijini.
Walimu Ma Jun na Ning Yi, waliotafsiri kitabu hicho wanafundisha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha SISU, pia katika Taasisi ya Taaluma za Afrika Mashariki ya SISU.
Tangu kuasisiwa kwake mwaka 2018, taasisi hiyo imefanya utafiti wa kina katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni za nchi za Afrika Mashariki, huku ikiwakuza wanafunzi wengi wanaojua Kiswahili na utamaduni wa waswahili.
Rais Xi Jinping alitoa hotuba yake kwenye Mikutano ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) iliyofanyika Beijing mwaka 2024.
Kwenye hotuba hiyo, alisema baada ya juhudi za pamoja za miaka 70, uhusiano kati ya China na Afrika umeingia hatua bora zaidi kihistoria.
Rais Xi alipendekeza kuimarisha zaidi uhusiano kati ya China na Afrika, na kujenga kwa pamoja Jumuiya ya China-Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja.
China na Afrika zinaafikiana katika kupata maendeleo na kukuza mambo ya kisasa.
Kuhusu mikakati ya kujenga na kudumisha amani, Mwandishi ametaja mila za utani katika sura ya mwisho ya kitabu hicho.
Utani ni uhusiano wa kindugu ulioko kati ya watu wa makabila mbalimbali ya Tanzania ambao unatokana na watu wa makabila hayo kuwa na uhusiano wa kivita, kibiashara na kadhalika.
Kwa kifupi, utani ni utamaduni wa amani wa makabila ya kibantu ya Tanzania, kwani kwa maoni ya mwandishi utani baina ya makabila ni mchango mkubwa wa watanzania katika dhana ya udumishaji wa utamaduni wa amani katika dunia.
Hivyo inahitajika utafiti zaidi ufanywe kuhusu Utani ili kuona jinsi ya kuendeleza falsafa hiyo kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Katika makala hii, Mwalimu wa lugha ya Kiswahili kutoka SISU, Ning Yi anasema kuchapishwa kwa Utamaduni na Maendeleo Nchini Tanzania kunatoa maudhui mengi ya kina kwa mawasiliano ya kitamaduni baina ya China na Tanzania.
Vile vile kunatia nguvu mpya katika mawasiliano ya kitamaduni baina ya China na Afrika.
Kitabu hicho kinarejea Tanzania kama mlango katika kufichua tamaduni tofauti na mchakato wa maendeleo ya jamii Barani Afrika.
Pia kinasaidia wachina kuelewa Afrika kwa mapana zaidi.
Vile vile mapendekezo ya ujumla ya kutekelezwa kwa sera za utamaduni katika kitabu hiki yanatoa mawazo na njia mpya kwa mawasiliano ya kitamaduni baina ya China na Afrika.
Mwandishi Song Yiting, Mwanafunzi wa Shahada ya Pili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:Yiting_Mo@126.com

Mwandishi Ning Yi ni mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:02706@shisu.edu.cn