Na Mwandishi Wetu
MWANZA: ‘’TANGU nchi yetu ipate uhuru tumekuwa tukitunga sheria kwa lugha ya kiingereza lakini zaidi ya asilimi 80 ya watanzania wanatumia lugha ya Kiswahili kama lugha mama,”
Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole amesema hayo wakati akizindua Kikosi Kazi maalumu cha Wataalamu Wabobevu wa Kiswahili nchini.
Wataalamu hao wametoka Chuo Kikuu Huria (OUT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM, Chuo Kikuu cha Dododma (UDOM) Baraza la Kiswahili (BAKITA) na wataalamu wa sheria waliokutana kwa lengo la kuhakiki Muongozo wa Ufasili wa Sheria na Istilahi za Kisheria zilizoandaliwa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Amesema, “Na tunapotaka kila mtu kufuata sheria maana yake lazima aijue na kuilewa vizuri lakini hawawezi kuilewa kama ipo kwenye lugha ambayo hawaijui huku tukitaka waifuate,
“Hivyo ufasili wa sheria utasaidia sana jamii kupunguza kufanya makosa kwa kujua masharti ya sheria wanayotakiwa kuzingatia haswa kwa kuwa kutojua sheria sio utetezi pale unapofanya makosa”.
Amesema kumekuwa na changamoto kwamba utekelezaji wa sheria umekuwa ni mdogo, uzingatiaji wa matakwa ya sheria umekuwa ni mdogo na wakati mwingine sio kwa sababu ya ukaidi ila ni kwa sababu ya lugha inayotumika kwenye sheria.
Amesema ufasili wa sheria utawawezesha wananchi wazijue sheria, wazizingatie ikiwa ni pamoja na kusaidia utekelezaji wa sheria hizo na utoaji wa haki.
Amesema serikali kwa sasa imeweka msukumo mkubwa kwenye kuhamasisha uwekezaji nchini lakini kumekuwa na migogoro kwenye maeneo mbalimbali kati ya wawekezaji na wananchi, ikifuatiliwa inaonekana wananchi hawaifahamu sheria inayosimamia uwekezaji husika.
Pia amesema msukumo huo huo umeelekezwa kwenye Mahakama za Tanzania kuendesha kesi na kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndio inayoeleweka na watu wengi.
Amesema kutokana na umuhimu huo ni lazima sasa kazi ya ufasili wa sheria ifanyike katika misingi ya ufasili inayofahamika kwa kila mtu na ndio maana umeandaliwa Muongozo wa Ufasili ili hata pale mahakama inapokutana na utata kwenye maeneo fulani ya sheria iliyofasiliwa wataweza kutumia muongozo huo kujua misingi iliyotumika kufasili sheria husika yenye utata.
“Pamoja na faida zote hizo lakini kubwa zaidi ni mahakama kutafsiri sheria na kutoa haki kwa Kiswahili katika utoaji wa haki na sheria kwa lugha ya Kiswahili pia kutasaidia kukuza demokrasia, uchumi, uwekezaji na maendeleo ya watu kwenye nyanja zote,” amesema.
Kwa maelezo yake, kukamilika kwa mwongozo huo, Istilahi za Kisheria pamoja na ufasili wa sheria kuu 446 za Tanzania kutasaidia jamii kuzielewa, kuzifuata na kupunguza kufanya makosa yanayotokana na kutojua kwao sheria sambamba na utoaji wa haki.
Vile vile amesema wamebaini wakati mwingine kwenye kutafsiri wanajikuta wanataka kubadili tungo za kiingereza ili zibaki maana ile ile na hivyo kujikuta haieleweki na haibebi yale masharti ya kisheria yaliyopo katika kifungu kilichopitishwa na Bunge.
Hivyo Mwongozo huo utawezesha kuwa na mfanano wa tafsiri.
Naye mmoja wa wajumbe wa kikosi kazi hicho ambaye ni mwandishi maarufu wa riwaya na kazi za sanaa, Profesa wa Sheria Abdalah Safari amepongeza jitihada kubwa iliyofanyika katika kuhakikisha kunakuwepo na Muongozo wa Ufasili wa Sheria nchini ili zieleweke kwa maana moja.
“Niipongeze sana Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kazi hii kubwa iliyofanyika maana baada ya Serikali kutoa tamko la kila sheria kutungwa na kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili itafanya watu wengi kujitokeza kufanya kazi hiyo japo kimsingi msimamizi mkuu wa jambo hilo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
“Sasa kutokana na uhitaji huo na watu watakapojitokeza kufasili sheria lazima kuwepo na mwongozo maalumu wa kuufuata kwenye kufanya kazi hiyo ili kuhakikisha watumiaji wa sheria hizo wanapata maana moja na sio maana tofauti na kuleta mgongano kwenye kutoa haki mahakamani,” amesema.
Profesa Safari ambaye pia ni Wakili, amesema baada ya ufasili huo ni muhimu kuwepo kwa kamusi ya sheria na maneno yake kwa lugha ya Kiswahili ili kuweza kutafsiri yale maneno ya kiingereza yanayotumika kwenye sheria na dhana zake kwa Kiswahili fasaha.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria Mstaafu, Sarah Barahomoka ambaye ndiye mwenyekiti wa kikosi kazi hicho amesema kazi hiyo wanayoifanya inaingia kwenye historia kwa kuandaa muongozo wa ufasili wa sheria nchini.
Ameahidi kuifanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa ili isaidie kuweka misingi ya ufasili wa sheria na katika utoaji wa haki na uelewa wa sheria kwa kila mtu.
Hayati Rais John Magufuli wakati akihutubia Bunge alisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa sheria kwa wananchi kwa kutunga sheria kwa lugha ya Kiswahili.
Katika kutekeleza azma hiyo, Mwaka 2021 Bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Tafsiri za Sheria ambapo pamoja na mambo mengine iliweka sharti la kwamba lugha ya sheria sasa ni Kiswahili na lugha ya kutumika katika vyombo vya utoaji haki nchini nayo ni Kiswahili.