Na Danson Kaijage
KILIMANJARO: SERIKALI imepeleka elimu ya fedha kwa wananchi wa Kata ya Makanya, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, itakayochochea maendeleo yao kiuchumi.
Elimu hiyo ya fedha inawalenga wananchi, wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima, wafugaji, watumishi wa umma na binafsi, watoa huduma za fedha kuwawezesha kufahamu sheria, kanuni na miongozo ya huduma ndogo za fedha.

Vile vile kufahamu masuala ya akiba, mikopo, uwekezaji wa fedha, bima, matumizi bora ya fedha na kujipanga na maisha ya uzeeni.
Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Dionesia Mjema, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha.
Vile vile kupanga bajeti, kuweka akiba, na mikopo salama.

“Matatizo mengi ya kifamilia hutokana na changamoto za kifedha, hivyo elimu hii itasaidia kuboresha maisha ya familia nyingi, na ndoa nyingi zinazovunjika hutokana na mzigo wa madeni.
“Nahimiza ushirikiano kati ya wanandoa katika kupanga matumizi ya mikopo,” amesema.
Diwani wa Kata ya Makanya, Damari Kangalu ametoa shukrani kwa Wizara ya Fedha kwa kuwapelekea mafunzo hayo muhimu, kwa kuwa elimu hiyo itawasaidia kuepuka mikopo umiza na kuimarisha hali yao ya kifedha.

“Hata wale wenye kipato kidogo wanaweza kuweka akiba na hatimaye kuwekeza ili kupata faida kubwa zaidi kwa muda mrefu. Hili litasaidia kuinua uchumi wa familia na jamii kwa ujumla,” amesema .
Ofisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Stanley Kibakaya, ameeleza kuwa wapo watoa huduma za fedha wasio waaminifu na hawatoa taarifa sahihi za huduma zao kwa wateja hali hiyo imesababisha watumiaji wengi kutojua wajibu wao na kusababisha migogoro kati yao.
” Hivyo kila Mtoa huduma ahakikishe kabla ya kutoa huduma wanatoa elimu ya fedha na kuweka wazi wajibu wa Mtoa Huduma na Mteja kwenye mkopo au huduma anayotoa,” amesema.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Makanya wamefurahishwa na mafunzo hayo yanayotolewa na Wizara ya Fedha pamoja na Taasisi zake kwa kuratibu elimu hiyo muhimu.
Mafunzo hayo yanatolewa katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro, zikiwemo Wilaya ya Same, Mwanga na Rombo.