Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: JAMII inapaswa kupewa elimu ya namna bora ya kuhifadhi takataka ili ziweze kutumika tena ama kuchomwa kutokana na aina ya taka husika.
Meneja wa Mradi wa Ustahimilivu wa Jiji la Dar es Salaam ( DURP), Dkt. Madaka Tumbo amesema hayo wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti uliofanywa kuhusiana na ukusanyaji taka.

Dkt. Tumbo amesema jamii inapaswa kupewa elimu juu ya namna mabadiliko ya tabia nchi yanavyoathiri ukusanyaji taka, utupaji wa taka, lakini ongezeko la joto ambalo linasababisha taka kuoza haraka.
Amesema kutokana na ongezeko la joto hilo, linasababisha taka kuoza haraka.
“Kutokana na taka kuoza haraka tunajaribu kuhusanisha mabadiliko ya tabia nchi na namna gani sekta nzima ya taka inahusika kuanzia taka zinavyotolewa, uzoaji hata zinavyotupwa.
Amesema,” Kwa sasa hivi masuala ya utunzaji wa taka na namna ya kukusanya, unatakiwa kutenganishwa.
Taka mbichi, taka ngumu, taka za plastiki tunabidi kujenga uwezo kwa jamii itenge takataka.

” Na hata wakatenga zinafanywa nini taka mbichi ziweze kuwa mbolea au kuwa chakula cha kuku na samaki. Pamoja na fursa hii bado hatujawa na uwezo mkubwa wa kupata hizo taka,” amesema.
Amesema kwenye mitaa pia kunapaswa kuwepo na maeneo yaliyotengwa ya kukusanyia taka zilizotengwa.
Naye Ofisa Mazingira kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Zanzibar. Jaco Abdalah amesema kuna tatizo katika suala zima la udhibiti wa taka, kwa kuwa kwa sasa taka zinazalishwa kwa wingi.

Amesema, ” Pia ongezeko la watu linaongezeka na idadi ya makazi inaongezeka, shughuli za uchumi zinaongezeka, shughuli hizo zinasababisha ongezeko la taka katika maeneo mbalimbali,”.
Amesema pamoja na ongezeko hilo, bado uwezo wa manispaa ni mdogo haujatosheleza kukusanya taka zote zinazozalishwa ikizingatiwa na uwingi wa taka na kiwango cha taka kinachozalishwa.
“Kwa sasa tunazalisha wastani wa taka tani 654 kwa siku, uwezo wetu zisizozidi tani 400 kwa kila siku,” amesema na kuongeza hali hiyo inasababishwa na uchache wa vifaa vilivyopo lakini pia miundombinu ya ukusanyaji taka.
Amesema kiasi kikubwa kinachozalishwa ni taka zile zina uwezo wa kuoza.
” Pia Tuna uwezo wa kutengeneza mbolea, mkaa, chakula cha kuku lakini bado hazijatumika vizuri,” amesema.
Amesema ujio wa mradi huo utahakikisha taka zinatumiwa vizuri, taka zile zinazooza na kuzalisha bidhaa nyingine zinaongezwa thamani ili kuboresha mazingira.