–Atoa Wito wa Uchangiaji Wenye Maadili Katika Uchaguzi Mkuu 2025
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ametoa ujumbe mzito kwa wanahabari nchini, akisisitiza nafasi ya vyombo vya habari katika kudumisha amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Dkt. Biteko ametoa ujumbe huo wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Amesema vyombo vya habari haviwezi kupuuzwa, akivifananisha na maji ambayo ni muhimu kwa kila mtu kila siku.
“Vyombo vya habari ni kama maji, usipoyatumia kuyanywa, utayatumia kuoga. Usipoyatumia kuoga, yatatumika kukumwagia ukizimia,” amesema Dkt. Biteko huku akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na sekta ya habari kwa maslahi ya kitaifa.
Katika hotuba yake yenye msisitizo wa uzalendo na maadili ya uandishi, Biteko ameonya kuwa bila umakini, vyombo vya habari vinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kijamii, kidini, au hata kisiasa.
Ametoa rai kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Tusipokuwa makini, wanahabari na vyombo vyao wanaweza kugawa taifa letu. Habari inaweza kuchochea migawanyiko ya kidini, kikabila au hata kuanzisha mivutano mikubwa,” amesemq Biteko.
Akitiliq mkazo hoja ya uvumilivu, Dkt. Biteko amesema tofauti za kimawazo si kosa, bali ni sehemu ya demokrasia, akitoa mfano wa mapenzi ya soka ambapo mtu anaweza kuipenda Simba au Yanga bila kubughudhiwa.
“Kama mtu anapenda Simba, aachwe aipende. Kama ni Yanga, vilevile. Hakuna kosa. Tujifunze kuvumiliana,” amesema kwa msisitizo huku akihimiza kuwa baada ya uchaguzi kila mmoja arudi kwenye nafasi yake ya kujenga taifa.
Mkutano huo uliowakutanisha wadau mbalimbali wa habari, usalama, na siasa, Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wanahabari dhidi ya kutoa taarifa zenye mlengo wa uchochezi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ameeleza kuwa uchaguzi ni kipindi nyeti ambapo kila mtu anapaswa kuheshimu sheria.
“Wajibu wetu ni kuhakikisha sheria zinasimamiwa kwa haki. Lakini tunawaomba wanahabari wawe makini – habari zenu ziwe za kujenga, si za kuchochea,” amesema.
Katika hatua nyingine Dkt Biteko amezindua rasmi Mfumo wa TAI HABARI – mfumo wa kidijitali unaotumiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari kusajili wanahabari nchini Tanzania.
Uzinduzi huo ulifanyika sambamba na mkutano huo, ukiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha uwajibikaji, uthibitisho wa weledi na maadili ya wanahabari nchini.
Mfumo huo unatajwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa changamoto za usajili holela wa wanahabari na utaleta uwazi zaidi kuhusu nani anaruhusiwa kufanya kazi ya uandishi kwa mujibu wa sheria.
Kwa ujumla, mkutano huu wa wadau umetoa dira na mwongozo thabiti kwa wanahabari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Msimamo wa serikali, kupitia kwa Dk. Biteko, umetuma ujumbe kuwa vyombo vya habari vina wajibu wa kulinda amani, kuimarisha mshikamano na kulisaidia taifa kufanikisha uchaguzi wa haki, huru na unaokubalika kwa wote.