Na Waandishi Wetu
Mnamo Septemba 2024, Kituo cha Vyombo vya Habari cha Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) huko Beijing kilikaribisha waandishi wa habari kutoka nchi mbalimbali.
Picha hii inaonyesha mwandishi wa habari kutoka Afrika (aliye upande wa kushoto) akizungumza na roboti ya kibinadamu (aliye upande wa kulia).
Roboti hii inaweza kutoa majibu kwa haraka na kutoa huduma za vyombo vya habari kwa ufanisi.
KADRI teknolojia ya akili bandia (AI) kutoka China inavyozidi kujengeka katika michakato ya maendeleo barani Afrika,
Pande hizo mbili zinafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiteknolojia, hivyo kuchochea mageuzi na maendeleo ya uchumi wa Afrika kwa kasi zaidi.
Bara la Afrika lina hazina kubwa ya rasilimali za data na masoko makubwa ya matumizi ya teknolojia, hali inayoonyesha uwezekano mkubwa wa maendeleo ya akili bandia.
Mwaka juzi 2023 idadi ya watumiaji wa kila mwezi wa programu za AI barani Afrika ilizidi milioni 40, huku bidhaa zinazohusiana na teknolojia hiyo katika soko la programu za simu zikipanda kwa asilimia 24 ukilinganisha na mwaka uliopita.
Kwa kutumia zana za uchakataji wa lugha kwa akili bandia (AI), taasisi za afya nchini Nigeria zinaweza kutafsiri zaidi ya lahaja 200 za maeneo mbalimbali kwa wakati,
Hivyo kuunda mazingira rafiki zaidi kwa lugha katika huduma za kliniki. Nchini Tanzania, mifumo ya AI katika kilimo hutumika kutoa mwongozo mahsusi wa kudhibiti wadudu waharibifu kwa mazao ya mihogo kwa kutumia picha kutoka setilaiti.
Mifano hii inaonesha mchango wa akili bandia katika sekta muhimu za maisha ya wananchi.
Hata hivyo changamoto za ukosefu wa teknolojia ya kisasa na uwezo mdogo wa matumizi bado zinahitaji kupatiwa ufumbuzi wa kina.
Uimarishaji wa mfumo wa ushirikiano wa kidijitali kati ya China na Afrika unaendelea kuwa msaada wa kimkakati katika kutatua changamoto hizo.
Julai mwaka jana, 2024 pande hizo mbili zilisaini Mpango wa Utekelezaji wa Ushirikiano wa Kidijitali, ambao umeweka msingi wa ushirikiano katika maeneo ya kisasa, kama vile akili bandia na mawasiliano ya quantum.
Takwimu zinaonesha kuwa kampuni za China zimechangia ujenzi wa kilomita 150,000 za mtandao wa mawasiliano na kilomita 66,000 za njia za usafirishaji wa data barani Afrika, kurahisisha upatikanaji wa intaneti ya kasi kupitia simu katika maeneo mengi ya bara hilo.
Miradi ya kimkakati kama vile Kituo cha Uhifadhi wa Data cha Serikali cha Misri na Warsha ya Luban nchini Kenya imeanza kutekelezwa kwa mafanikio.
Kituo cha Misri ambacho ni cha kwanza cha AI katika Afrika Kaskazini, kinatoa zaidi ya huduma 200 za wingu, huku warsha ya Kenya ikijikita katika kukuza vipaji vya ndani kupitia mafunzo ya teknolojia ya AI.
Miradi hii inaonyesha dhahiri mbinu shirikishi ya maendeleo ya pamoja ya miundombinu na rasilimali watu.
Chini ya mwongozo wa sera, ushirikiano wa China na Afrika katika AI sasa unapanuka kutoka ngazi ya miundombinu hadi katika mnyororo mzima wa viwanda.
Mfano wa hili ni Kituo cha Data cha Misri, kilichojengwa kwa ushirikiano wa Shirika la Uhandisi wa Nishati la China, na Huawei pamoja na Kituo cha Ujuzi wa Kidijitali cha Kenya, kinachoendeshwa na Chuo cha Ufundi cha Tianjin.
Miradi hiyo inaonyesha ushirikiano wa kina wa sekta mbalimbali, zikiwemo uzalishaji, elimu na utafiti.
Maendeleo ya kasi ya China katika Akili Bandia — ikiwemo mafanikio ya hivi karibuni kama uvumbuzi wa Deepseek, yameziletea nchi za Afrika fursa mpya za uhamishaji wa teknolojia.
Katika Mkutano wa Kilele wa FOCAC 2024, Mpango wa Hatua 10 za Ushirikiano ulipitishwa, ukilenga utekelezaji wa miradi 20 ya mageuzi ya kidijitali,
huku kuanzishwa kwa Kituo cha Ushirikiano wa Teknolojia ya Kidijitali kati ya China na Afrika kikitarajiwa kuimarisha na kukuza zaidi ushirikiano wa kiteknolojia kati ya China na Afrika.
Kwa kuangazia mustakabali wa ushirikiano huu, pande zote mbili zimeweka mkazo katika maeneo matatu muhimu.
Utafiti na maendeleo ya kiteknolojia, ushirikiano wa viwanda, na ukuzaji wa vipaji. Kupitia ujenzi wa mfumo endelevu wa ushirikiano wa kidijitali,
China haitachangia tu kuisaidia Afrika kuvuka vikwazo vya mabadiliko ya kidijitali, bali pia itachochea matumizi mapya ya teknolojia ya China.
Ushirikiano huu, unaojengwa juu ya misingi ya usawa, kuheshimiana na manufaa ya pande zote, unazidi kuwa njia yenye maana ya kujenga Jumuiya ya Kiwango cha Juu kati ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja.
Mwandishi Ning Yi, mwalimu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:02706@shisu.edu.cn

Mwandishi Song Yiting, mwanafunzi wa shahada ya pili kutoka Chuo Kikuu cha Taaluma za Kimataifa cha Shanghai (SISU).
Barua pepe:Yiting_Mo@126.com