Na Mwandishi Wetu
Antananarivo, Madagascar: MKUTANO wa 45 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza rasmi leo, Agosti nne, 2025, jijini Antananarivo, Madagascar, kwa kuanza na Kikao cha Wataalamu cha Maofisa Waandamizi kinachojadili utekelezaji wa Mpango Mkakati Elekezi wa Maendeleo wa Kikanda wa mwaka 2030 (RISDP 2030).
Kikao hicho muhimu kimefunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi, ambaye amesisitiza haja ya kufanya tathmini ya kina ya utekelezaji wa RISDP, sambamba na kubaini vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya miradi ya pamoja ya kikanda.

“Licha ya mafanikio yanayoonekana katika utekelezaji wa RISDP, bado kuna changamoto zinazohitaji mshikamano wa pamoja baina ya nchi wanachama. Tunahitaji kuongeza kasi ya utekelezaji, hasa katika miradi ya miundombinu na biashara ya ndani ya ukanda,” amesema Balozi Chimbindi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mtendaji wa SADC anayeshughulikia Ushirikiano wa Kikanda, Angeles N’Tumba, ametoa wito kwa nchi wanachama kubuni mbinu za kudumu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya RISDP.

Amependekeza kujifunza kutoka kwa jumuiya nyingine kama ECOWAS, ambayo imefanikiwa kuanzisha mifumo endelevu ya kutafuta rasilimali za maendeleo.
Mkutano huu wa SADC unatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa kisera na kiutekelezaji wa malengo ya RISDP, huku ukisisitiza mshikamano wa kikanda kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ujumbe wa Tanzania katika kikao hicho unaongozwa na Mkurugenzi wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Talha Waziri, ambaye pamoja na wajumbe wengine wa nchi wanachama, wanashiriki katika mapitio ya kina ya utekelezaji wa RISDP ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi unaotarajiwa kufanyika Agosti 17, 2025.
